Jumanne, 5 Agosti 2014

NAMNA YA KUBADILI MAUMIVU YA MAPENZI KUWA FURAHA

BILA shaka mpenzi msomaji umzima buheri wa afya na muda huu unanifuatilia katika busati letu zuri la mahaba, mahali tunapojuzana na kuelimishana mambo kadha wa kadha yahusuyo mapenzi na uhusiano. Nakukaribisha kwa moyo mkunjufu tuijadili mada yetu ya leo kama inavyojieleza hapo juu.
Ni ukweli usiopingika kuwa katika zama hizi za sayansi na teknolojia, maumivu ya mapenzi yameongezeka maradufu. Kile tunachoamini kuwa ni maendeleo, kinazidi kuzitesa hisia na nafsi zetu na suala la kutendwa, kuumizwa, kuvunjika mioyo au kusalitiwa, linaonekana kuwa fasheni siku hizi.
Kinachowasumbua wengi ni kushindwa kuelewa nini cha kufanya baada ya kuangukia katika dimbwi la maumivu ya kimapenzi. Hebu kila mtu ajiulize:
Umewahi kukuta SMS ya mapenzi kwenye simu ya mpenzi wako akimtumia mtu mwingine tofauti na wewe? Ulijisikiaje uliposikia mtu mwingine akiitwa majina mazuri ya kimapenzi  na mpenzi wako, pengine kuliko hata yale ambayo huyatumia kwako? Ulichukua uamuzi gani?
Kila mtu ataeleza anavyojua yeye lakini ukweli ni kwamba wengi hawajui kukabiliana na maumivu hata yale yanayosababishwa na maisha ya kawaida. Kwa kuwa maumivu, usaliti, kuvunjika kwa mioyo na uongo katika mapenzi ni jambo ambalo kwa kiasi kikubwa halikwepeki katika zama hizi, jambo la msingi ni kujua nini cha kufanya baada ya kutokewa na dhoruba hizo za kimapenzi.
Hebu msikilize msomaji wangu, Jane wa Ilala Bungoni jijini Dar, alivyokuwa analalama:
“Wiki nzima inaisha sasa, siendi kazini, chakula hakipandi, usingizi sipati wala sitamani kitu chochote, kitu pekee ninachokifanya ni kulia usiku na mchana, naomboleza na kulalama katika kila sekunde inayopotea mpaka natamani kujiua, sioni tena thamani ya kuishi, nayachukia mapenzi, nawachukia wanaume,” alisema Jane huku akilia kutokana na kutendwa na mwandani wake aliyemsaliti kwa kutoka na rafiki yake kipenzi.
Yawezekana Jane hayuko peke yake, wapo wengi ambao wanateswa sana na mapenzi lakini hawana sehemu ya kuyatoa maumivu yao, wanaumia ndani kwa ndani, miili yao inadhoofika kila siku, hawana furaha japokuwa wanapata mahitaji yote muhimu, chanzo kikuu kikiwa ni mapenzi.
Hapo ndipo ninapoona umuhimu wa kila mmoja kujua namna ya kusimama tena pale anapoangushwa na maumivu ya kimapenzi.
Zifuatazo ni mbinu ambazo zitakusaidia kuyabadilisha maumivu yako ya kimapenzi kuwa furaha.

JIFUNZE KUSAMEHE NA KUSAHAU
Hakuna jambo ambalo hutuliza fikra na hisia za mapenzi kama kukubali kumsamehe yule aliyekuudhi kabla hata hajakuomba msamaha na kuamua kusahau yote yaliyotokea. Yawezekana wengi mtasema haiwezekani. Inawezekana na wote waliojaribu mbinu hii walifanikiwa.
Marafiki, lazima kila mmoja aelewe kwamba unapokasirika au kuumizwa, anayeteseka siyo yule aliyekusababishia maumivu bali ni wewe mwenyewe. Hasira au maumivu ya kimapenzi huwa kama moto mkali ambao huitafuna taratibu nafsi ya mhusika.
Ukisamehe maana yake unaupa moyo na akili yako nafasi ya kupata sehemu ya kutulia na kuuzima moto ambao tayari ulishaanza kukolea ndani yako.


Hisia za kuumizwa katika mapenzi kwa mwanaume hazitofautiani na za mwanamke,,wote wanaumia

Katika mapenzi kwa asilimia kubwa wanawake huwa wanaona wenyewe ndiyo wanaumia sana linapotokea  suala la usaliti katika mahusiano aliyonayo, lakini ni wazi kabisa hata wanaume wanaumia sana kwahiyo usifikiri mwanamume akisalitiwa hawezi kuumia hapana kwani hata yeye ni binadamu inapotokea ametendwa basi lazima ataumia ijapokuwa maumivu yanatofautiana,, mwanamke anaweza kuonyesha wazi maumivu anayoyapata lakini mwanamume akawa anaumia moyoni huku akijionyesha usoni kuwa hajaumia kumbe anaumia sana. kwahiyo naweza kusema maumivu ya mapenzi hayaangalii mwanamume au mwanamke inategemea na wewe ulipenda kwa kiasi gani.

maumivu haya hutokana na vitu vingi ikiwemo kukosa uaminifu, kuachana au kuachika nk,,na kutokana na maumivu haya hupelekea baadhi ya watu kujuta kupenda,, kuapa kutopenda tena,,na hata kunywa sumu na kushindwa kufanya kazi kwa ufanisi. Muhimu ni kuzingatia suala la mapenzi ya dhati na kuishinda tamaa,,hakuna anayependa kuumia katika mapenzi kwahiyo basi kama hupendi kuumizwa usimuumize pia mwenzio,,,kwasababu kuna wengine ni mahodari kuwaliza wenzi wao kila kukicha. Tubadilike jamani mimi naamini hakuna kinachoshindikana